Jubilei ya miaka 25
YA MISIONI YA TANZANIA
25.09.1990 – 25.09.2015
Tunamshukuru Mungu kwa
sababu ametulinda na kutuongoza hadi kufikia siku ya leo kuanzia tarehe 25
septemba 1990 siku ambayo tulifika hapa Tanzania.
Mwaka huu utakuwa hasa ni mwaka wa shukrani kwa Mungu, ambaye ametupatia neema
nyingi, nguvu za kushinda shida, miito, ulinzi, msaada mbalimbali na wafadhili.
Tumsifu na tumshukuru Mungu kwa sababu chochote kilichofanyika ni kwa sababu
Yeye amefanya; tumsifu na tumtukuze Mungu kwa sababu Yeye tu anayeweza kufanya
mambo haya ya ajabu.
Kwa msaada wa Mungu, jubilei yetu inaingia ndani ya mwaka wa watawa na
ndani ya jubilei ya miaka 150 ya kuzaliwa kwa Mama Mwanzilishi.
Natumaini kwamba sisi sote, katika mwaka huu wa jubilei, tutaweza kufurahia na
kuimarisha wito wetu ili tuweze kuendelea kufanya utume wetu kwa ari mpya na kwa
furaha, hivyo kuwatangazia wengine kwamba Mungu tu ndiye aliyetuita,
anayetuongoza na anayetusaidia katika safari yetu.
Daima tufurahi na tumshukuru kwa sababu Mungu ni Mkuu na anatutendea mambo makuu!
Sala ya jubilei ya miaka 25
Sala kwa ajili ya Jubilei ya miaka 25 tangu ilipoanza Misioni yetu ya Tanzania
Ee, Mungu, Bwana na Baba yetu tunakushukuru kwa kazi ya mikono yako,
kila kitu tunachokiona ni tuzo kutoka kwako, zawadi ya Maongozi yako.
Tunakushukuru kwa ajili ya wale wote ambao wameshiriki katika ukuaji wa Misioni hii.
Kila siku Wewe umetutangulia katika kila kazi na kwa upendo wako umefanya Misioni yetu iwe bustani nzuri sana, machoni pa watu wengi.
Sisi sote tunakushukuru!
Yote uliyotuahidi umeyatimiza kwa nguvu ya uwepo wako, na ya Upendo wako wa kibaba.
Sisi sote tunakushukuru!
Uangalizi wako wa Baba mwenye upendo umeimarisha nguvu zetu na ari yetu ya kukutumikia
Sisi sote tunakushukuru! Wewe unaendelea kuiangalia na kuitegemeza kwa njia ya Roho wako Misioni yetu kwa sababu uliijenga kwa ajili yako mwenyewe kama sehemu ya baraka Sisi sote tunakushukuru! Bwana, kila kitu ni zawadi yako, hatuna chochote cha kukurudishia isipokuwa makosa yetu na udhaifu wetu. Tunakuomba msamaha Bwana, kwa sababu hatujakurudishia chochote kinacholingana na upendo wako mkubwa na neema zako nyingi. Ee Bwana usiiache kazi ya mikono yako! Endelea kulibariki Shirika letu na Misioni yetu kwa kutupatia miito mingi na mitakatifu na pia endelea kutusaidia kutimiza kwa uaminifu ahadi tulizokuwekea. Tunakuomba si kwa mastahili yetu, kwa sababu hatustahili, bali kwa mastahili ya Kristo Yesu Mwanao. Kwa maombezi ya Bikira Maria Bibi wa Misioni yetu, ya Mtakatifu Yosepu mhasibu wetu, mt. Ursula, fanya ili sisi sote tuisikie leo nguvu ya enzi yako, ya utukufu wako juu ya Misioni yetu na juu ya kila mursula wa Tanzania. AMINA