Masista wa UrsulaESPANSIONE-descrizione in lingua italianawa Tanzania

 

HISTORIA YA MISIONI


 

Tukipenda kueleza historia ya Misioni ya masista Wa-ursula hapa Tanzania ingekuwa vizuri kuongea juu ya :

Historia ya mwonekano wa upendo wa Mungu katika Misioni ya Wa-ursula Tanzania.

Tangu mwanzo Mungu ametutangulia kwa uwepo wake katika kila hatua, katika kila mipango, na pia kwa uwepo wake na  msaada wake Mungu,  tumeiona neema yake iliyokuwa juu yetu, na bado ipo  pamoja nasi wakati wa kutambua vizuri mambo gani anayopenda sisi tuyafanye ….Mungu alitusaidia  kutambua  pia namna ya kuishi,  kwani wakati tulipopata  wazo la kuja Tanzania hatukuwa na kitu chochote.

Kwa njia ya ushauri ya P. Bukeke Conrad wa Jimbo la Shinyanga ambaye alikuwa masomoni Italia na aliyekuwa akiishi  katika nyumba yetu ya Roma, na pia  kwa ruhusa ya Mama Mkuu Ursula F. sr Rita pamoja na sr Jolanta, mwezi Aprili 1985 walisafiri kwenda jimboni Shinyanga ili kuongea na Askofu wa mahalia  na kuona ni kwa namna  gani masista waursula wangeweza kufika kufanya utume katika Jimbo lake. Safari ilikuwa ngumu …

Lakini Mungu  alikuwa na mpango mwingine!

Sr Maria Fiorillo, mdogo wake sr Rita,  wa Shirika la masista wa Abuduo Damu ya Yesu, aliyekuwa akiishi nchini Tanzania kwa miaka mingi, alimshauri dada yake kuanzisha Misioni katika Jimbo la Singida, mahali walipokuwa wakifanyakazi  Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ili mapadri waweze kulisaidia Shirika hasa katika mwanzo mgumu wa uanzishaji wake.

Sr Rita aliupokea ushauri wa mdogo wake na hivyo mwezi januari mwaka 1987 alisafiri tena  kuja Tanzania pamoja na sr Jolanta ili  kuongea na wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu waliokuwa wakifanya utume katika jimbo la Singida.

Tulianza kukutana na marafiki na watu mbalimbali  katika nyumba zetu na kuwaeleza mipango yetu ya kufika Tanzania. Baada ya hapo tulianza kusali  na kuuza vitu mbalimbali tukijaribu kukusanya fedha za kuanzisha Misioni ya Tanzania.

Fedha iliyokusanywa katika siku tatu za sala kilipatikana kiasi kile kile kilichotosheleza kulipia ticket ya safari ya msichana wa kwanza kutoka Tanzania ambaye alipaswa kufika Italia kwa ajili ya kupata malezi ya kitawa:  sr Maria Teresa Tesha.

Hii ilikuwa ishara kwetu kwamba Mungu alipenda  Misioni yetu ianze!

Tungeweza kuwa na hofu ya kuondoka Italia na kuanzisha Misioni Tanzania tukiyakumbuka maneno ya Mama Mkuu  aliyesema kwamba Shirika halina fedha ya kujenga nyumba,  wala fedha kwa ajili ya kuishi Tanzania, wala masista wa kuanzisha Misioni Tanzania.

Watu wengi wangeweza kufikiri kwamba haikuwa  busara kuanzisha Misioni  pasipo msaada wowote kutoka katika  Shirika….lakini wakati Roho anavuma haiwezekani kuipinga nguvu yake.

Mama mkuu alisema: “ Shirika halina fedha ya kujenga nyumba”…lakini Mungu alitupatia nyumba  kwa njia ya msaada wa chama cha “WORLD LABORATORY”,  nyumba ya kuhamishika iliyotengenezwa na mabati, iliyotoka Italia, vipande vipande na ndio iliyojengwa hapa Mkiwa kwa haraka ndani ya mwezi mmoja ili masista waweze kupata nyumba ya kuishi.

Alisema pia “Hatuna fedha za kuwapa ili kuishi Tanzania!” Lakini fedha haijakosekana na hatuna wasiwasi kwamba Mungu hayupo kwa sababu tunayaona Maongozi yake  yakifanya kazi kila siku. Alisema pia “Hatuna masista wa kutuma Tanzania“, lakini Mungu kwa mpango wake wa ajabu aliijenga jumuiya ya kwanza: Masista wawili kutoka Italia na masista watatu kutoka Tanzania ( hawa walienda Italia kama wasichana na huko walipata  malezi ya utawa na walibaki hadi kufikia kuweka nadhiri.)

Tarehe 2 mwezi wa tisa 1990 masista wawili wa-Italia  walipata msalaba wa kimisionari parokiani  huko Roma na tarehe 24 mwezi wa tisa 1990 walianza safari kwa ndege na kushuka  Dar es salaam tarehe 25 mwezi wa tisa 1990 walishuka  Dar es salaam. Tarehe 27 septemba walifika Itigi (Singida) kule  ambako walipata nyumba ya kuishi. Waliishi kati ya nyumba za madaktari ambao wanafanya kazi katika hospitali ya Mt. Gaspari Itigi. Mpaka sasa  masista ambao wanafanya kazi katika hospitali hii wanaishi katika  nyumba moja kati ya nyumba hizo.

Mwaka 1991 tulianza kufanya utume katika kijiji cha Mkiwa katikati ya wenyeji wa mahalia, ingawa hata wakati tukiishi Itigi, kila wiki, tulifika Mkiwa kutoa msaada wetu tukipeleka dawa na nguo na pia tukisafisha eneo letu na kuondoa visiki. Tulianza pole, pole, kuingia katika mazingira mapya na kuishi kwa namna  ambayo ilikuwa ni ngeni kwetu. Katika kipindi cha mwanzo cha kukaa Mkiwa tulielewa kwamba ili kuingiza Karama yetu kati kati ya watu, tungepaswa kuwapenda, kuishi kama wao, kutoa nguvu zetu zote na  muda wetu kwa ajili yao. Wanakijiji wa Mkiwa walisubiri kutoka kwa Wa-ursula: matumaini, misaada mbalimbali, faraja na huruma.

Wote walihitaji watu  ambao wangeweza kuongea nao Kuhusu  Mungu kwa sababu mapadri wamisionari walikuwa wakifika   mara moja tu kwa mwezi ili  kuadhimisha Misa. Hii haikutosha  na bado haitoshi hata leo kwa sababu watu wanamuhitaji mtu ambaye anaweza kuwasaidia kutatua matatizo na  shida mbali mbali za maisha yao

Misioni tangu mwanzo ilikuwa marejeleo kwa ajili ya wale waliohitaji chochote: Chakula, nguo, fedha za kwenda hospitalini, kukopa kwa ajili ya ada za wanafunzi …na pia sanda za kuzikia marehemu.

Tulipofika  Mkiwa tuliwakuta watu ambao  mateso, njaa na machozi vilikuwa urithi wao lakini  walikuwa na  tunu nyingi na sisi tulijifunza mengi kutoka kwao.

Walikuwa  watu ambao waliweza kutoa mfano wa umaskini wao, wa tabasamu na mfano wa  kupokea mapenzi ya Mungu bila kulalamika. Walikuwa ishara ya  uchungu wa Moyo wa Yesu Mteswa ambao kwa neno lake “ Naona kiu” na pasipo  nguo msalabani  alisubiri kutoka kwetu bilauri moja ya maji.  Walikuwa mfano wa  Yesu msulibiwa ambaye kwa macho yaliyojaa machozi alisubiri kutoka kwetu jibu moja.

Misioni yetu ilikuwa  katika sehemu maskini pale ambapo watoto walikuwa wakitembea bila viatu na pia walivaa nguo zilizochanika. … pale ambapo vijana walihitaji kuongozwa, kulelewa na kupata ushauri  ili  kupata maisha mazuri ya baadaye na yenye mafanikio.

Katika kijiji hiki cha Mkiwa tarehe  21 novemba mwaka  1991 tulifungua nyumba yetu ya kwanza kwa ajili ya  kuwapokea wasichana ambao walipenda kujiunga na shirika: Nyumba ya Mt. Ursula

Tarehe moja mwezi wa januari 1992 tulikabidhiwa  ufunguo wa nyumba ile ya kuhamishika iliyojengwa kwa vipande vya  mabati.  Hatukuwa na sehemu ya kusali, tulikuwa tukikutana kusali kwenye  baraza ya ile  nyumba ya mabati na wakati wa kipindi cha mvua vitabu vya masifu vililowana.

Ufunguzi rasmi ya misioni  ulifanyika  tarehe 24 juni 1992.

Mungu amewaalika  Wa-ursula kuingiza Tanzania karama ya Moyo wa Yesu Mteswa, aliwasaidia kwa neema yake na kwa nguvu zake ili waweze kuzishinda shida mbalimbali walizokutana nazo. Mungu aliwatuma kwao kwa mfululizo wafadhili kutoka sehemu mbalimbali za Italia, na misaada mbalimbali kutoka jumuiya za shirika letu duniani.

Tulipofika Mkiwa tulianza utume wetu hasa kulea  watoto na vijana, kulingana na  karama yetu. Tuliwakusanya watoto na vijana, tukaanzisha  vyama mbalimbali vya kitume, pia tulianzisha mafundisho ya  katekismu ili kuandaa vijana na wakatekumeni kupokea  sakramenti mbalimbali za Kanisa

Tarehe 19 mwezi wa tatu 1993 tulifungua shule ya chekechea na sehemu kwa ajili ya kupata chakula kila siku.

Kabla ya sisi kuingia Mkiwa hakukuwa na  zahanati  kwa hiyo wagonjwa wote walilazimika  kutembea kwa miguu mwendo wa  kilometa kumi na zaidi ili kupata huduma ya matibabu.

Ili kuwasaidia wagonjwa kwa huduma hii ya afya tulifungua  zahanati iliyojengwa  ndani ya  nyumba ya kuhamishika (ya mabati)

Desemba 1993 Baba Askofu Bernardo Mabula Askofu wa Jimbo la Singida, alilibariki Kanisa letu la kwanza. Tulipoingia  Tanzania yeye alitupokea kwa maneno haya: “Njooni, maskini wanahitaji msaada wenu”

Kwa mara ya kwanza mwaka 1993 tuliweza kusherekea Sikukuu ya Noeli katika kanisa letu, pamoja na watu wa kijiji cha Mkiwa. Usiku ule wa Noeli walifika kanisani watu mbalimbali, wakatoliki na wasio wakatoliki yaani waislamu na waumini wa madhehebu mengine. Usiku huu ulikuwa ni usiku wa sala na furaha kubwa ambao hatuwezi kuusahau.

Kuanzia siku ile tulianza kugonga kengele ya “Sala ya malaika  wa Bwana” ambayo mpaka sasa  tunaendelea kugonga..  Sala ya “Malaika ya Bwana” inawaalika watu kusali sio tu  masista,  bali hata wakristo wa Mkiwa ambao wanapenda kusali pamoja nasi.

Mwezi septemba 1994 Mhashamu Baba Askofu Bernardo Mabula, Askofu wa Jimbo Katoliki Singida alibariki jengo la Novisiati yetu ya kwanza mbele ya Mama Mkuu wetu Ursula F.,  mbele ya manovisi, mbele ya wasichana wa malezi ya  kitawa na mbele ya wakristo wa Mkiwa. Walipokelewa manovisi  7 na baada ya miaka 2 wao waliweka nadhiri za kwanza tarehe 14 septemba 1996, walikuwa masista sita.

Kijiji cha Mkiwa kina uoto wa kisavana, kiko umbali wa mita 1300 kutoka usawa wa bahari. Ardhi yake ni kavu yenye kiu kama watu wa mahali hapo walivyo na kiu.

Wakati tulipoingia Mkiwa hakukuwa na umeme wala maji hivyo tulikwenda kuchota maji bwawani. Kwa hiyo haikuwa rahisi kupata maji katika maeneo haya. Hata unapochimba kisima , mara nyingi yanapatikana maji yenye chumvi. Kisima cha kwanza ambacho tulichimba kilikauka baada ya miaka mitatu…

Lakini Bwana ambaye hatuachi  peke yetu hata siku moja, alituzawadia kisima kingine cha maji mengi na ya kutosha na kwa hiyo kimeweza kutuhudumia hadi sasa kwa miaka 21.

Wakati tulipoanza kutoa visiki katika eneo la shamba letu la kulima, watu walicheka na walisema kwamba tunatoka jasho bure kwani eneo lile ni la kichanga sana haliwezi kuota chochote.

Lakini jangwa limeota  maua!

Yote ni matendo makuu ya Mungu! Njoni mkaone mambo makuu ambayo Mungu tu ameweza kuyatenda! ( zab.65)

Kwa upande wa mawasiliano,  kulikuwa na tatizo kubwa kwani hata barua za Mama Mkuu alizokuwa akiandika zilichukua muda hata wa  miezi mitatu kutufikia na kama zilikuwa barua za sikukuu zilifika baada ya sikukuu. Kwa kweli hili lilikuwa ni tatizo kubwa na ilikuwa vigumu kupokea.

Tunamshukuru Mungu, leo tuna umeme wa Tanesco, umeme wa solar na pia mtambo wa internet unaofanya kazi kwa njia ya satelait. Mtambo huu wa mawasiliano tulizawadiwa na rafiki yetu mmoja ambaye alifanya kazi bure katika Misioni yetu kwa mwaka mmoja. Tunamshuku Mungu!

Kadiri idadi ya watawa ilivyozidi kuongezeka tulianza kubuni namna ya kujitegemea kwani hakukuwa na maduka karibu ya kununulia mahitaji yetu. Kwa hiyo tulianza kufanya pia shughuli mbalimbali kama: kupanda miti,  kulima bustani, kulima na kupanda mahindi, maharagwe na alizeti na pia kufuga wanyama mbalimbali kama ng’ombe, nguruwe, mbuzi, kondoo n.k.

Pia tulianza kujenga nyumba kubwa ya kutosha ili tuweze kuwapokea wasichana waliopenda kujiunga na Shirika letu.

Leo bustani ni kubwa kwa sababu tulipata zawadi kutoka wafadhili aina ya mabomba ambayo hutumika kumwagilia kwa matone madogo madogo.

Leo tunayo pia miti ya migomba, machungwa, na ya matunda mbalimbali kama mapapai, maembe, mastafeli na maua ya aina mbalimbali.

Tunaandaa pia  miche ya kuuza.

Leo hii ndani ya miaka  25 hapa  Mkiwa tuna nyumba zifuatazo:

Nyumba ya masista, novisiati, nyumba ya wageni, jiko, ukumbi wa mikutano, maktaba, makanisa mawili, moja la kuadhimisha Misa hata na wakristo wa Mkiwa na moja kwa ajili ya kuabudu. Tuna  shule ya chekechea, zahanati, ukumbi wa maendeleo, mashine ya kusaga, sehemu ya kuwapa wazee chakula, shule ya ufundi, sehemu ya kufinyanga vitu vya udongo, Hosteli ya wanafunzi wasichana wa  shule ya sekondari ya Mkiwa.

Pia kuna Grotto la Bikira Maria na baada ya Grotto mwishoni mwa shamba kuna msalaba ambapo ndani yake kuna kaburi la sista mmoja wa kwanza ambaye amezikwa humo.

Ndani ya kipindi cha miaka 25 tunamshukuru Mungu tumeweza kupata miito na kwa hiyo tumeweza kufungua jumuiya 14 katika majimbo mbalimbali ya Tanzania

“Asante Mungu”