Masista wa UrsulaESPANSIONE-descrizione in lingua italianawa Tanzania

 

Furaha ya Mama Ursula Tafakari ya padre Carlo Calori


 

Kuna furaha gani leo katika jamii yetu? Hasa katika kuishi kwetu?

Mtu wa leo anahisi sana njaa ya furaha, ana njaa ya kuwa na maisha yenye maana na yenye matumaini. Mara nyingi mtu anaogopa kujionesha kama mtoto… na anaogopa hata kusema kwamba Injili ni “Habari Njema.” Je, leo inawezekana kuongea juu ya furaha? Je, leo inawezekana kupatikana furaha wakati dunia imetawaliwa sana na umasikini na dhuluma?

Lakini ili tuishi kama wafuasi wa kweli wa Injili hakuna njia tofauti na ile ya kuwa mashuhuda wa “utakatifu wenye furaha”. Ukweli haina maana ya kufanya mipango mbalimbali ya kuinjilisha pasipo kushuhudia upendo kwa ajili ya uhai na kufanya mazoezi ya kuwa watu wenye furaha. Watakatifu wengi wameelewa kwamba daima tunapaswa kuwa na furaha kwa sababu sisi sote ni watoto wa Mungu. Kati ya watakatifu Mt. Ursula Ledòchowska Mwanzilishi wa masista Waursula wa Moyo wa Yesu Mteswa, ana nafasi ya pekee. Huyu mama, miaka michache kabla ya kifo chake alisema: “ Mungu ni Baba yetu, kwa hiyo kile ambacho kinatokea, katika maisha yetu, kutoka kwake ni kizuri.”

Mama Ursula ni kati ya Watakatifu ambao wameleta furaha duniani. Yeye ameandika hivi: “Mungu alipenda kutakasa watu kwa njia ngumu ya msalaba. Lakini kwetu sisi Mungu ametuachia kazi ya kuwasaidia watu katika njia ya msalaba, tukipanda kando kando yao mionzi midogo ya jua la furaha. Tunaweza kufanya hivyo mara nyingi kwa tabasamu ambalo linawaambia watu upendo na wema wa Mungu.”

Kuhusu Mama Ursula wote waliomfahamu walisema kwamba alikuwa ni mtu mtaratibu, mpole, mtulivu, mwenye furaha, na daima alikuwa tayari kuwasaidia wengine.

Ursula Ledòchowska ametoa fundisho moja la matumaini duniani, kwamba mambo yote yatakuwa mazuri tukimtanguliza Kristu.

Tangu utoto wake walimwita “Mionzi ya jua” kutokana na wema wake, na uwezo wake wa kuwafariji watu na kwa sababu alikuwa menye furaha wakati alipowatumikia watu katika shida zao mbalimbali.

Yeye aliendelea kuwa na tabia hii kwa maisha yake yote.

Mama Ursula daima alikuwa mfano wa furaha na wa mtu mwenye kukubali mapenzi ya Mungu.

Kama Mungu apendavyo ” ulikuwa ndiyo msemo wake.

Yeye alikuwa mlezi mwenye ari tulivu, mtume na mmisionari huko Urusi, mpendwa ekumeni katika nchi za Skandinavia. Yeye alianzisha mtindo mpya wa kuishi maisha ya kitawa yenye ufukara, kiasi na uwezo wa kupokea aina mbalimbali za maisha. Yeye aliweza kuunganisha pamoja karama ya malezi na upendo kwa ajili ya waliohitaji zaidi. Na Mama Ursula aliishi hivi ingawa alikuwa na mahangaiko mengi na shida mbalimbali.

Pamoja na kuwa na mahangaiko mengi, furaha ya injili ilishinda daima.

Tunaweza kujiuliza kwa nini Mama Ursula daima alirudia moyoni mwake maneno ya Mtakatifu Paulo, “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini?” (Waefeso 4:4).

 

1. Sababu ya kwanza ni ya kiteolojia

 

 Pengine utajiuliza kwa nini Mama Ursula alikuwa na utulivu daima? Ukweli ni kwamba yeye alikuwa na imani sana. Tukiangalia maisha ya Yesu, tunaona kwamba dhambi ilimsikitisha sana, tazama alipokuwa pale bustanini jinsi alivyopata uchungu wa mateso. Kweli Yesu alisulibiwa, lakini sasa amefufuka, ameyashinda mauti na dhambi zote. Kwa hiyo, kuwa katika furaha daima, ni tendo la imani katika Ufufuko wa Yesu. Yesu ni asili ya Ufufuko wetu, ni Yeye ambaye anageuza misalaba yetu na maisha yetu yote.

 

2. Sababu ya pili ni ya kisaikolojia

 

 Huzuni yetu inatokana kwa kuona kwamba ulimwengu hauheshimu imani yetu na utumishi wetu. Au huzuni yetu na kutojisikia kwetu vizuri kunatokana na sababu kwamba sisi tunafanya mipango yetu, yenye akili na yenye faida…baadaye hali na matukio ya maisha na ya historia vinafanya kwamba mipango yetu inakuwa haina maana tena na haiendelei vizuri kwa hiyo inakuwa vigumu sana kuamini kwamba Mungu anaongoza maisha ya binadamu.

 Ni muhimu kwa hiyo kuishi kwa matumaini ya kikristo. Maana yake ni kuwa na hakika kwamba Bwana atatusaidia daima na hakuna kitu kitakachopotea kwa sababu Bwana anakumbuka yote na anaiona thamani ya kila kazi hata kama ni ndogo na hata kama matokeo ya ile kazi sio kama tulivyopanga na tulivyotamani, bali ni matokeo ambayo Mungu ameyapanga.

 Maisha ya mama Ursula yalijaa mambo kama haya na yeye aliyapokea akiamini neema na mwongozo wa Mungu

 Kwa hiyo…” furahini katika Bwana”.

 

3. Sababu ya tatu ni upendo

 

 Jamii iliyokata tamaa na yenye huzuni hujaribu kuficha huzuni yake katika anasa. Ushuhuda wa furaha ya kweli ni msukumo na tegemeo.

 Mama Ursula aliishi daima siri hii na ameiacha kama urithi wenye thamani kwa watoto wake. Ameandika: “watu wanalalamika daima kwamba leo haiwezekani kukutana na mtu mwenye uso mtulivu na wenye furaha…kipindi hiki ni kigumu sana na usoni mwa watu wazima na hata mwa watoto, mahangaiko na wasiwasi vimeacha muhuri wa huzuni na ghairi. Kama ilivyo wakati wa baridi binadamu anahitaji joto na mwanga wa jua, hivyo wakati huu mgumu watu wanautafuta uso mtulivu, wenye furaha, unaoangaza…”

 

Kwa hiyo chemchemi ya furaha ya mama Ursula ni

Imani

Matumaini

Upendo