WOSIA


IX.

AGIZO LA TISA

KUJIHINISHA

 

        

Watoto wangu, tafakarini mara kwa mara Moyo Mtukufu wa Yesu uliochomwa kwa mkuki, uliovalishwa taji la miiba. Sikilizeni yale malalamiko ya uchungu ya Kristo Mteswa: "Nimetafuta wa kunituliza lakini sikupata". Tafakarini ule moyo ulioneshwa dharau, fedheha, mateso na mtaelewa kwamba anayeupenda ule Moyo anapaswa kuelewa kujinyima na kitu ambacho kimeuunganisha kabisa: upendo wa msalaba.

Msifikiri kuwa mnatakiwa kujinyima sana na kufanya vitubio vikubwa zaidi ya kawaida. Hapana, hapana watoto wangu! Mimi, katika wito wetu, niko mbali kabisa na mtindo wowote usio wa kawaida, lakini nawashauri kujinyima kile kinachotokana na kazi zetu na umaskini wetu. Nawasukuma kwa kujihinisha yale tunayokutana nayo kila siku, ambayo ni ya lazima katika kufanya vizuri kazi zetu, yale tunayohitaji ili kuishi kwa uaminifu katika upendo na katika utii wa kitawa. Ningesema, kujinyima kile cha ukarimu ambacho hakionekani kwa macho, hakivutii uelekevu wa watu kwa hiyo ni wa uhakika zaidi, kwa sababu hakileti vishawishi vya upuuzi vya kujisikia wema kuliko wengine. Maisha ya kitawa yanapaswa kuwa maisha ya kujinyima. Maisha bila kujihinisha sio maisha ya kitawa.

Kujihinisha kwa kwanza, watoto wangu, ni kuwa waaminifu katika kuitekeleza Katiba yetu. Katiba yenyewe bila shaka ni mzigo kwetu sisi na kwa hiyo ni kujihinisha. Tuwe waangalifu wenyewe wa kutokosa amri za Katiba pia huku ni 29

kujihinisha thabiti. Waalimu wa maisha ya ndani ya kiroho, wanatuhakikishia kwamba maisha ya mtawa anayetimiza kwa uaminifu Desturi takatifu ni maisha ya kishahidi. Kabla ya yote fanyeni kujihini huku.

Fanyeni kwa hiari huku kujinyima kutokana na vitendo vya kila fadhila. Hakuna fadhila bila kujinyima. Mama mmoja maarufu sana mama wa ki-katoliki, Madame Svétchine, alisema kwamba fadhila ambayo haina ugumu siyo fadhila.

Kujinyima ni kifo cha pole pole kwa asili yetu ya ubinadamu, ni kuishi kinyume cha nia zetu, uthamani wetu, mapenzi yetu, kwa kulikanyaga neno "nataka" na "sitaki", katika kutimiza zaidi kile kinachompendeza Mungu.

Msicheze cheze na mahinisho, kujinyima mambo madogo ya kitoto, na kuacha kufanya yale ya kweli yanayoleta fadhila. Lakini ukijinyima hata kwa mambo madogo ukifanya kwa upendo wa Mungu, unapata faida kwa roho yako, ikiwa huyaondoi yale ya maana ambayo ndio yanaleta wema wa kweli. Wengi wanabuni mahinisho madogo madogo wakijisikia baadaye huru kutofanya yale mahinisho ambayo yapo katika kuishi, katika kazi na katika maisha ya jumuiya. Hata kama hayo ya kwanza ni mazuri, haya ya mwisho ni ya maana zaidi na ya uhakika zaidi kwa sababu hayatupeleki kwenye upuuzi. Fanyeni mazoezi ya uhodari katika kujinyima katika yale ya maana zaidi, ambayo ni sehemu kamili ya mazoezi ya kila wema.

Unahitaji kujihinisha ili kuishi kwa ulinganifu na umoja pamoja na masista, yaani kuwa daima tayari kusaidiana kwa ukarimu. Unahitaji kujihinisha ili kusali vyema kwa mkazo wa fikra, kufanya kazi kwa juhudi, kutii kwa utayari na ujasiri, na kuweza kuushika moja kwa moja utulivu wa moyo. Hizi nafasi huhitaji kuzitafuta; zinajileta zenyewe ikiwa wewe uko tayari kuzitumia. 30

Kujihinisha kwingine ni kuvumilia kimya kimya na kwa hiari misalaba midogo ambayo Mungu anatupatia: ni upendo wa msalaba. Maisha yanaleta, mara kwa mara, msalaba wake mkubwa zaidi, bali kila siku kuna misalaba midogo, kama sindano, ambayo yote hayo ni maumivu na uchungu moyoni. Yapokeeni kwa mikono wazi, watoto wangu, hii misalaba midogo. Mungu ndiye anawatumieni. Misalaba ni wonyesho la mapenzi yake. Tuipende kwa moyo wetu wote sababu inatuongoza kwa Mungu na kwa uhakika zaidi tutapata faraja kubwa. Na mbele ya misalaba mikubwa inayojaza maisha yetu uchungu na mateso, pigeni magoti kama Mtakatifu Andrea mkisena: "Salamu msalaba mtakatifu, matumaini yangu ya pekee, Salamu!".

Jaribio zuri zaidi la upendo ambalo tunaweza kutolea kwa Mungu, ni kuweza kuchukua kwa hiari misalaba yetu. Hakuna upendo mkubwa zaidi ya huo. Itakuwaje usiupende msalaba unaotusaidia kusema kwa Mungu: Bwana wewe unaona kwamba nakupenda!

Pendeni kila msalaba, mdogo au mkubwa uwao wowote, na hata ule msalaba mdogo ambao labda utakuwa kwenu, yaani kifo cha mzee Mama yenu. Pendeni misalaba yenu midogo, kila mmoja wa hii ni masalio matakatifu ya msalaba wa Kristo na kwa hiyo twapaswa kuushikilia kwa upendo na kuuchukua kwa furaha takatifu.

Misalaba ambayo Mungu anatupatia, midogo au mikubwa, ni shule nzuri zaidi ya kujihinisha. Kupokea misalaba kwa hiari, kimya kimya, kwa utulivu, huku ndiko kujitoa kunakopokelewa zaidi na Mungu; hatuwezi kufikiri chochote kingine cha maana zaidi. Kwa hiyo, iweni na juhudi wanangu wapendwa: semeni daima kwa furaha: "Salamu Ee msalaba mtakatifu, tumaini langu la pekee!".