WOSIA
VIII.
AGIZO LA NANE
IBADA KWA BIKIRA MARIA
Katika huu wosia wangu napaswa kuacha baadhi ya kurasa kwa ajili ya Mama yetu, Malkia na Bibi, Maria Mtakatifu.
Mpendeni Maria, mpendeni kwa upendo, mpendeni kweli kweli kama watoto wema, mpendeni huyu Mama yetu. Tumepewa yeye kutoka kwa Mungu. Yesu juu ya msalaba ametuachia Maria kama urithi. Mapenzi ya mwisho ya Yesu ni kwamba sisi tuwe watoto wema wa Maria. Kwa hiyo tuelewe hivyo, tusali ili tuwe watoto wema wa Maria na tujaribu kwa nguvu zetu zote kuwa hivyo. Maria kweli ni Mama mwema na mwenye huruma. Yeye anatamani ukombozi wetu zaidi kuliko sisi tunavyotamani. Kwa hiyo mkimbilieni yeye kwa imani kama watoto. Msiruhusu kamwe kwamba kunajificha mioyoni mwenu hali ya kukata tamaa, na hali ya ukosefu wa matumaini. Kuweni na uhakika kwamba Maria, kwa kuwa ni msaada wenu, atawafanyia muujiza kuliko kuwaacheni. Kama mtoto ambaye yuko kwenye mikono ya mama yake, hivyo hata ninyi, bakini kwenye miguu ya Maria kwa amani, hata japokuwa wakati mwingine dhoruba itawakumba.
Pendeni kile kimpendezacho Maria. Pendeni Rozari. Msiiseme tu kwa maneno, bali kwa maisha yenu yote, mkijiingiza kwenye fadhila za Maria zilizoelezwa kwenye mafumbo ya Rozari. Kusali Rozari kiwe ni kitendo cha juhudi na upendo kwa Maria, iwe ni kuweka juhudi kwa wema wake, iwe ni kutafakari kwa moyo juu ya uaminifu katika kuufuata mfano wa Maria, iwe ni sala ya kupata utakatifu kutokana na utakatifu wa Maria. Kuweni daima na Rozari pamoja nanyi,
27mchana na usiku, msiiache kamwe. Iwe ni rafiki yenu mwaminifu, mnyororo wa kuunganisha moyo wenu na moyo wa Mama yetu mbinguni.
Na yawe haswa ya thamani maneno ya Maria yaundayo neno rasmi la Shirika letu: "Tazama mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema" (Lk.1:38). Jaribio la upendo mkubwa kweli kwetu kwa Maria ni kuziiga fadhila zake. Pendeni basi kama yeye, ambaye ni mtakatifu na msafi, kuwa waaminifu watumishi wa Bwana, daima kuwa tayari kuyatimiza mapenzi yake, yawe yanaleta furaha na starehe au yawe yanaleta misalaba na uchungu. Mapenzi ya Mungu! Kama Maria alivyokuwa akisalimu kila matamko ya mapenzi ya Mungu kwa maneno: "Tazama mimi ni mtumishi wa Bwana...", aliyoyasema yeye siku moja na kuyarudia katika maisha yake yote, kwa moyo na kwa matendo, hivi hata ninyi watoto wangu, muwe kama yeye daima, katika matukio mbalimbali ya maisha, watumishi wanyenyekevu wa Bwana wanaoyapokea daima mapenzi ya Mungu, kwa vyovyote vile, kwa tabasamu mdomoni, kwa "Fiat"( iwe kwangu kama ulivyosema) na "Deo gratias"(tumshukuru Mungu) moyoni, hata kama tuna machozi machoni - kama Bikira Maria.
Na kama mapenzi ya Mungu yakiwaelemea kwa uchungu mkali, na hata kama mtakosa nguvu ya kuvumilia kimya kimya, basi inueni macho ya mioyo yenu kwa Maria, kwa Mama yenu mwenye huruma na ombeni: Ee, Mama utufundishe kuwa wakimya daima watumishi wa Bwana, wanoatamani kitu kimoja tu: Mapenzi ya Mungu yatimie na sio yetu yatimizwe.
Mpendeni Maria, watoto wangu, pendeni Rozari na niaminini: Upendo bora zaidi kwake ni ule wa kuwa kama yeye wakimya, waaminifu, watumishi wanyenyekevu wa Bwana wanao rudia
28mara kwa mara kwa moyo na kwa matendo: Tazama, na yatimizwe kama Mungu apendavyo, kama Mungu apendavyo!