WOSIA


VII.

AGIZO LA SABA

UPENDO KWA MSALABA

 

          

"Lakini mimi sitajivunia kamwe kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristu; maana kwa njia ya msalaba huo ulimwengu umesulibiwa kwangu, nami nimesulibiwa kwa ulimwengu"

( Wagal. 6:14 )

Wanangu wapenzi, kwa mtawa, ibada kwa Yesu msulibiwa inapaswa kuwa kiini cha maisha yake yote ya ndani, kiini cha roho yake. Kumbukeni kwamba kutoka katika mti mtakatifu wa msalaba ndipo zilipotiririka ibada zote muhimu katika maisha ya mwanadamu. Yesu msulubiwa, kwa mateso na kifo chake, ametustahilia neema juu ya neema: Ekaristia Takatifu. Kwa kweli Misa Takatifu ni tendo la kutimiza tena sadaka ya Yesu msalabani. Juu ya msalaba Yesu aliwaacha wautoboe moyo wake ili kuufanya uwe makimbilio, ulinzi na mbingu ya roho, uwe pia kwa ajili yetu chemchem ambapo zinamiminika neema na upendo. Juu msalabani Yesu ametupatia Maria kama Mama yetu na ametukabidhi kwa Maria kama watoto. Juu msalabani zilishuka neema kwa watakatifu, neema ambazo ziliwatakatifuza na zimewafanya wao waweze kuwa waombezi wakubwa na mifano halisi ya fadhila na utakatifu.

Chochote kile kilicho kizuri, kitukufu na kitakatifu katika maisha yapitayo ya kawaida kimeshuka kutoka kwenye msalaba kwa sababu Kristo ametustahilia yote hayo kwa mateso yake na kifo chake. Na kwa hiyo watu waliojiweka wakfu wanapaswa kuinua macho yao kuelekea msalaba, kama ua lielekeavyo jua. Katika msalaba upo wokovu wetu, katika msalaba yapo matumaini yetu, katika msalaba upo upendo na 24

furaha, na kwa huo tunapata kila jema. Kwa sababu juu msalabani Yesu ametukomboa kwa Damu yake Takatifu, ametufungulia milango ya mbinguni; kwa mateso yake ametuhakikishia furaha ya milele.

Ni upendo kiasi gani, ni shukrani kiasi gani tunapaswa kutoa kwa Mkombozi wetu! Ulimwengu unafikiri kidogo kuhusu shukrani hizi, unawaza kidogo kuhusu huo upendo, kwa sababu wenyewe unadai upendo kwa upendo sadaka kwa sadaka; kwa sababu msalaba unaonekana kutufanya tutafiti na kuutuliza Moyo mteswa wa Kristo, tunapaswa kuchukua pamoja naye huo msalaba, kwa sababu masikitiko yake na machozi yake hayaendani na furaha ya juu juu ya ulimwengu. Kwa hiyo baadhi ya watu – waliojiweka wakfu kwa Mungu – kwa namna ya pekee wanao wajibu wa kumpenda Yesu Msulibiwa, wa kumfariji kwa upendo wao, wa kukaa miguuni kwake kama Maria Magdalena, wakibusu kwa upendo mkubwa vidonda vyake vitakatifu. Kwa nadhiri takatifu tumepigiliwa kwenye msalaba na tunao wajibu wa kumfuasa Yesu Msulibiwa – kuwa maskini pamoja na Yesu maskini, kuwa wachovu pamoja na Yesu mchovu, msalabani pamoja na Yesu Msalabani.

Kwa mtawa, msalaba ni furaha yake yote, ni upendo wake wote, ni chochote kile chake. Mtawa ameuacha ulimwengu na vyote ambavyo ungeweza kumpatia, badala yake amepokea msalaba na katika huu anapata kile ambacho anaweza kutamani:

„ Ee, msalaba utakuwa moyoni mwangu

makao yangu,

utajiri,

wewe utanifanya kuiona mbingu karibu zaidi.

Upendo, uhuru, kumbukumbu ya zamani na ya baadaye,

yote yanapatikana katika msalaba." 25

Hivyo shikilieni msalaba. Katika msalaba tafuteni furaha, faraja na kitulizo katika mahangaiko, mwanga kwenye giza, ushauri kwenye mashaka, majuto kwenye maanguko, utulivu kwenye dhoruba ya maisha, matumaini kwenye kukata tamaa, furaha wakati wa kifo!

Wanangu wapendwa, mpendeni Yesu Msulibiwa, mpendeni kwa moyo wenu wote. Jishikeni kwenye miguu yake, bakini na Yeye kwa mawazo na kwa moyo. Tafakarini mara kwa mara Mateso ya Bwana. Jifunzeni kwa Yesu msulibiwa jinsi ya kumpenda Mungu, jinsi ya kuwapenda wanadamu, jinsi ya kuwa wanyenyekevu, watii na wenye kujitolea, jinsi ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine, jinsi ya kufanya kazi kwa ajili ya utukufu wa Mungu na kwa ukombozi wa dunia. Njia bora zaidi ya kumtuliza Yesu msalabani ni kumwonesha upendo wako haswa, na kuiga fadhila zake.

Kadiri mtakavyo jaribu kumuiga Yesu msulubiwa, kadiri mtakavyo kuwa karibu zaidi na msalaba, ndivyo zaidi Msalaba utakuwa ni kila kitu kwenu duniani. Hata wakati wa Misa, tafakarini mateso ya Kristo. Fanyeni kwa hiari Njia ya msalaba, busuni mara kwa mara msalaba kwa upendo mkubwa na jifunzeni kwa urahisi kwamba katika msalaba kuna furaha kubwa - furaha ya mbingu katika machungu ya ulimwenguni.

Kwenye kanisa kuu la Mt. Maria wa Malaika – huko Roma - nimeyakuta maneno yafuatayo - ambayo yamekuwa katika maisha yangu kitulizo kikubwa, mwanga na utulivu - na nayatoa kwenu:

"Kwenye miguu ya Yesu

miiba ni waridi

kuteseka ni furaha,

kufa ni shangwe »