WOSIA
II.
AGIZO LA PILI
UNYENYEKEVU
Watoto wangu wapenzi, angalieni unyenyekevu wa Moyo Mtukufu na muufuate.
Sisi, wafuasi wa Moyo wa Yesu tunapaswa awali ya yote, kufuata hii fadhila yake pendelevu.
Sisi watumishi wa maskini, tunapaswa kuwa wadogo, wadogo sana, ili kuwavutia kwetu na kuwapeleka watu kwa Mungu.
Rudieni kila siku, sio tu kwa maneno bali kwa undani wa moyo: "utufanye wadogo kama yule mdudu mdogo anayetambaa chini, kwenye udongo, ambaye bila kufahamu miguu ya mtoto inamkanyaga bila kuogopa".
Muwe wadogo na msipende kuwa hivi kwa sababu fulani tu, sababu maono na kujisikia kwetu mara nyingi kunatudanganya, bali kwa maisha na kwa vitendo maana katika vitendo ndipo penye ukweli.
Jaribuni kuwa wanyenyekevu na wadogo.
Kumbukeni kuwa unyenyekevu ndio mzizi wa kila fadhila; fadhila ambayo haitokani na mzizi huu sio fadhila, hata kama inaonekana hivyo kwenye macho ya wanadamu.
Eleweni umaskini wenu na udhaifu wenu kuwa hauoneshwi kwa maneno wala kwa kujisikia, bali kwa vitendo. Msiseme: „tuko wadogo", bali tendeni kama wadogo.
Awali ya yote msichukiane na yeyote, wala kwa sababu ya aina yoyote. Mnyeyekevu hachukii kwa sababu anakubali kustahili kudharauliwa na anafikiri kuwa wote wanamtendea mema mno, kwa hiyo badala ya kuchukia anashukuru kwa kila jambo.
Wanangu msichukiane! Likataeni kama kishawishi, wazo litakalowachafueni, linalowaweka pembeni, linalowakosesha
9heshima na kujisahau ninyi. Ni kisingizio cha udhaifu kinachofanya tuachane na amani takatifu ambayo wanaifurahia wanyenyekevu. Hata wakiwafanyia mabaya semeni ninyi wenyewe kuwa, bado yote ni mazuri mno kwa sababu mngestahili motoni.
Shukuruni kwa kila jambo, na kamwe wanangu wapenzi, mnapaswa kuacha kutawaliwa na tabia za maelekeo. (hisia)
Kumbukeni kwamba mnyenyekevu hukubali na hupokea maonyo, hajitetei hata kama hayo maonyo sio ya haki. Mnyenyekevu anaamini kwamba wengine wanaona zaidi yake, na anatafuta kupata faida kwa yale maonyo anayopewa.
Mnyenyekevu hazungumzi juu yake mwenyewe wala kwa mema wala kwa mabaya.
Jaribuni kuzamisha kimya neno "mimi". Piganeni hadi mwisho dhidi ya tamaa ya makuu kwa sababu katika hayo ndio mwanzo wa kuanguka kwa mtawa. Katika hayo kunazaliwa magonjwa mabaya ya kiroho: kama vile chuki na wivu, ambayo yanaua maisha ya ndani.
Kuweni na tamaa moja tu: kuwa si kitu, msio wa maana, mkipita katika ulimwengu huu kama vile hampo.
Furahini kwa ajili ya maendeleo ya wengine katika kazi, wakati wanapata heshima kuliko ninyi, wakati kazi waliyopewa ni ya maana zaidi na ya juu zaidi.
Bakini watulivu pembeni kwenu, mkikumbuka kile tu kinachowashauri kitabu cha "Kumfuasa Kristo": "Unapenda kufahamu kitu kiletacho amani kubwa? Kutofahamika na kuonekana kuwa si kitu.
Ni amani gani inayokaa katika moyo wa mnyenyekevu! Achaneni na fikra za kujidhania wenye haki na hivyo kutoa hukumu kwa wengine.
Utapoteza nini ukikubali jambo linalotokea kwa wengine? Isipokuwa wakati ukikubali unaweza kuingia wewe mwenyewe
10au wengine katika hatari ya dhambi, nyenyekeeni kwa moyo, kwa jinsi inavyowezekana, katika mapenzi ya wengine.
Katiba yetu inasema "nyenyekeaneni wenyewe kwa wenyewe"; na katika huo, kuna unyenyekevu mmoja na kamili. Kupenda kuwa chini ya wote ni majaribu ya unyenyekevu wa kweli, ambao unamfanya mtu ajifikirie kuwa mdogo na wa chini zaidi kuliko wengine.
Watoto wangu, msitamani kamwe cheo au kazi ya hali ya juu na pokeeni kwa unyenyekevu, iwapo Bwana atawapeni, lakini msitamani kamwe. Furahini kama walio wadogo zaidi wataitwa kuzifanya.
Tiini kwa hiari wakubwa wenu hata kama ni wadogo zaidi, mkionyesha kwao heshima ile mliyokuwa nayo kwa mkubwa wenu wa Novisiati.
Watoto wangu wapendwa, kuweni wanyenyekevu, msitafute kusifiwa wala kufahamika. Kadiri mtakavyopokea kidogo kutoka kwa watu, ndivyo zaidi Mungu atakavyowazunguka kwa utukufu wa mbinguni.
Pendeni, watoto wangu, kuwa wadogo, wadogo sana; nafasi iliyo na uhakika zaidi ni ile ya mwisho. Jifunzeni kwa Moyo wa Yesu ambao ni mpole na mnyenyekevu. Kuweni wakimya kwa ndani na kwa nje.
Msipige kelele, ongeeni kwa sauti ya chini, tembeeni na fanyeni kazi kimya kimya. Kelele daima, hata kama pasipo kufahamu, ni kupenda kusema kwa watu wote kuwa: nipo mimi. (ni mimi)
Watoto wangu, nawaomba: kuweni wakimya na wanyenyekevu. Mungu atakuwa pamoja nanyi na Moyo Mtukufu hakika atabariki kazi zenu na upendo mtakatifu utawaunganisha.
Wanangu, kuweni wakimya na wanyenyekevu. Unyenyekevu ni fadhila ya pekee, msingi wa Wa-Ursula wa Moyo wa Yesu.
Nawaomba, watoto wangu, kuweni wanyenyekevu.