WOSIA


XIV.

AGIZO LA KUMI NA NNE

MKAZO WA FIKRA NA UKIMYA

 

Kama mnapenda wanangu kuwa karibu na Mungu, karibu na Yesu wenu; mnaweza kujizoeza kuwa na mkazo wa fikra na kuwa waaminifu katika ukimya. Ukimya ni amani ya roho. Wakati mnapofanya kazi zingatieni ukimya kulingana na aina ya kazi mnayofanya, zungumzeni kile cha maana, lakini msizungumze kile kisicho cha maana. Heshimuni ule ukimya mkuu kama matayarisho ya komunyo takatifu. Kuwe na ukimya kabisa katika sehemu ya klausura. Na inapokuwa ni lazima kuzungumza, zungumzeni, kwa sauti ya chini, ili msisumbue ukimya wa wengine, ili wasije wakatoa mawazo yao kwa Mungu.

Mwisho wa kazi zenu, wakati kengele inapogonga ili kukaa kimya, yanaanza maisha yetu pamoja na Mungu. Inua kadiri uwezavyo moyo wako kuelekea mbinguni. Ingia katika ule ulimwengu mtukufu. Pale wanakungoja Yesu na Mama yako Mtakatifu, malaika mlinzi, na roho nyingi zinazokupenda. Zungumza na wakaaji wa Mkoa wa mbinguni. Omba, shukuru, tolea masumbuko yako, woga na matumaini, kwa Moyo mpenzi wa Yesu na kwa Moyo wa Maria.

Furahi na vuta kwa mapafu yaliyojaa ile hewa ya umilele inayokuzunguka. Ni vyema kujitoa, hata kwa muda mfupi, kutoka duniani. Oh ni vema sana!

Na wakati wa mchana wakati kazi zimetusonga sana, wakati mwingine unapaswa kuzungumza zaidi ya ulivyopenda, na ni shida kuunganika na Mungu kwa sababu inakupasa kufikiria kazi ile ambayo umepewa, kwa hiyo jaribu kila wakati, kuuelekeza moyo wako kwa Bwana, kwa kumwambia kuwa 42

unampenda, kwa kufanya upya nia nzuri kwamba kila unachokifanya unafanya kwa kumpendeza Yeye tu. Kwamba maisha yako yote, kila kazi yako ni kwa Yeye tu, kwa Yeye peke yake.

Huku kuinua moyo kumwelekea Mungu, wakati mwingine, kunabadili kazi kuwa sala, na maisha yako ya duniani kuwa maisha yasiyo ya dunia bali ya utukufu. Usifikiri kufikia huo mkazo wa fikra na kuunganika na Mungu ni kwa muda mfupi tu. Hapana, ni kazi ya miaka mingi. Asubuhi weka azimio: wakati wa mchana au wakati mwingine, kwa mfano wakati unatoka katika sehemu moja kwenda nyingine, utaweza kuinua moyo wako kwa Mungu. Wakati wa kujihoji dhamiri yako jiulize kama umetimiza hiyo ahadi na weka tena ahadi hii.

Omba neema ya kuunganika na Mungu. Fanya kazi bila kukata tamaa, hata kama huoni matokeo. Pole pole, pasipo wewe kutambua, moyo wako utaunganika daima zaidi na Mungu, na Kristo atakuwa daima zaidi kiini cha maisha yako. Jaribu kuunganika na huo mkazo mtakatifu wa fikra, ukikwepa kupayuka kusiko na maana na uchunguzi usio na maana.

Kwa nini ufahamu yote? kadiri unavyofahamu kidogo yale yatokeayo karibu nawe, ndivyo zaidi itakuwa rahisi kwako kuhifadhi mawazo pamoja. Usijiingize katika mambo ya wengine hivyo utaepukana na wasiwasi mkubwa, na unaweza kufanya kazi na kusali kwa utulivu."Ni voir ni etre vue, ignorer et etre ignorée". (« Msitafute kuona, kuonekana, wala kufahamika kuweni msiojulikana »)

Ni furaha kwa roho inayoishi maisha haya. Sahau ulimwengu, jisahau haswa wewe mwenyewe. Ishi kimya kimya kwa ajili ya Yesu tu, katika yeye na pamoja na Yeye. Utafikia hiyo mbingu kama hapa duniani utajizoeza kwa uvumilivu na saburi, katika ukimya na katika fikra.