WOSIA


XI.

AGIZO LA KUMI NA MOJA

MAPENZI YA MUNGU

 

      

Ulimwenguni hakuna cho chote kikubwa zaidi ya mapenzi ya Mungu. Kanuni takatifu ni nzuri sana kwetu kwa sababu zinatuongoza, kuyatimiza mapenzi ya Mungu katika kila hatua. Lakini zenyewe zinaweza kujionesha hata kwa njia mbalimbali.

Katika Kanuni takatifu Mungu anatuonesha mapenzi yake kupitia njia mbali mbali za maisha, ambazo hazilingani na njia zetu, anatuonesha mapenzi yake ili tuweze kuyafuata na kujinyenyekeza kwa yenyewe. Kama tunapenda kuunganika kabisa na mapenzi ya Mungu, tunapaswa kuyatimiza si kwa uaminifu tu, bali kuyatimiza na kujinyenyekesha kwa yenyewe. Tunapaswa kuyakubali hata kabla hayajajitokeza, kwani kitu chochote ambacho Mungu anapenda kutimiza kwetu, anakifanya daima kwa ajili ya mema yetu. Tuishi kwa usalama katika mapenzi ya Mungu tukipigana dhidi ya wasiwasi, mahangaiko, woga, kwa wakati mwingine, hasa katika hatari na mateso yanayotokea ghafla. Haya mapenzi ya Mungu yana nguvu zaidi. Kwa nini wafadhaika? Kwa nini unahangaika? Itakuwa kile Mungu apendacho, na itakuwa vyema.

Kama Mungu apendavyo!

Kama tunayatamka haya maneno kwa upendo, yenyewe ni faraja kwa roho iliyo na uchungu. Yarudieni wakati mkiwa na fadhaa, yarudieni wakati Mungu anapowapatieni misalaba. Kwa hiyo sio tu kukubali mapenzi ya Mungu bali jinyenyekesheni kwa yenyewe kimya kimya, bila kulalamika, kwa tabasamu mdomoni, na kwa "Deo gratias"- yaani „Tumshukuru Mungu- ndani ya moyo. Kama Mungu apendavyo! 34

Huu msalaba ni mapenzi ya Mungu na mapenzi ya Mungu ni hazina yetu kubwa duniani, ni furaha ya moyoni inayompendeza Mungu. Kama Mungu apendavyo!

Pendeni mapenzi ya Mungu, kanyageni kwa uhodari lile ganda gumu na chungu la tunda ambalo Mungu amewapeni. Na mtajikuta mmeingia katika kiini cha mapenzi yake, chenye wema na utamu.

Mwanangu, unapenda kuunganika kabisa kwa undani na Mungu? Yatimize kwa uaminifu mapenzi yake, yakubali kwa upendo, nyenyekea kwa yenyewe kwa uhodari na furaha, na hivi utajiunga katika ncha ya utakatifu. Sala, kitubio, upendo- ndizo zilizo katika mstari mkubwa wa maisha ya kitawa. Kumbuka kwamba:

o Sala iliyo bora zaidi: ni kujiweka kwenye mapenzi ya Mungu.

o Kitubio kilicho bora zaidi ni kujiweka kimya kimya katika mapenzi ya Mungu.

o Upendo ulio mkubwa zaidi ni kuyatimiza kwa uaminifu mapenzi ya Mungu.

Kama Mungu apendavyo! Kama Mungu apendavyo! Kwa maneno haya mdomoni utaishi maisha ya utulivu hata kwenye dhoruba; furaha hata kwenye shida, upendo hata penye chuki, mtakatifu kwenye dhambi, mtukufu ungali bado duniani.

Kama Mungu apendavyo!