Wosia


MAAGIZO YA MZEE KWA WATOTO WAKE WAPENDWA

Watoto wangu wapendwa, ninyi mnafahamu ni jinsi gani ninavyowapenda na kadiri ulivyo katika moyo wangu wema wa roho zenu. Ningependa kuwaachieni baadhi ya mashauri ambayo yanatoka katika moyo wangu wa kimama na uliojaa upendo ili yawasaidie kufuata ile njia ambayo Mungu mwenyewe, kupitia hali mbalimbali, ametutayarishia sisi, amelitayarishia Shirika letu.

Nikiandika huu wosia wangu sio labda, kwa wazo langu, ninaonyesha ukosefu wa unyenyekevu, nikimuiga, kwa namna fulani, Mama na Mwanzilishi wetu Mtakatifu Angela?

Nimeshikwa na huo woga, lakini upendo nilionao kwenu umeshinda.

Linarudi kwa dhati wazo la kuwaachieni kama wosia wangu, mawazo yangu, kwa hiyo niko tayari kwa kazi hiyo katika Jina la Bwana.

Wanangu wapenzi, haya maneno ya Mama yenu mzee ambaye ninyi mnampenda kidogo yatakuwa muhimu kwenu, nina hakika, yatawasaidia baadhi yenu kutenda yaliyo mema. Na hata kama katika moyo wa mtu mmoja yatawasha cheche za upendo kwa Mungu, hii italeta furaha kubwa kwangu.

Kwa kila namna naandika kwa nia njema, kwa upendo mkubwa kwa Mungu na kwenu, watoto wangu. Kwa hiyo nategemea kwamba Bwana atapokea mapenzi yangu mema na atabariki kazi yangu.

Wanangu wapenzi, Bwana awe nanyi!

Namkumbatia na kumweka moyoni mwangu kila mmoja wenu, na kwa kila mmoja naomba msamaha kwa maudhi, ambayo labda kwa udhaifu wa kibinadamu nimeyafanya na kwa mifano 4

mibaya ambayo labda kwa wakati mwingine nimewaonesha, kwa namna yangu ya kutenda ambayo daima imekuwa sio sawa na kile nilichosema na hiki ambacho nawaandikieni sasa.

Nawaomba kwa unyenyekevu, mnisamehe kwa yote mkifahamu upendo wa kimama ambao ninao kwenu, ingawa mimi mwenyewe si mkamilifu, upendo unanisukuma kuwaona ninyi watakatifu na wakamilifu.

Kwa utakatifu wenu na wema wenu mlipie kwa Mungu ukosefu wangu wa utakatifu na wema. Kwa namna hii wanangu wapenzi mtashiriki katika utukufu wa Mungu na mtafupisha muda wa toharani wa Mama yenu mzee ambaye anatamani sana kuunganika mapema na Bwana.

Kwa herini wanangu, daima nitawaombeeni, na katika Moyo wa Kristo nitakuwa karibu nikiunganika nanyi. Mama yenu mzee hataacha kusali kwa ajili yenu ili tukutane siku moja wote pamoja mbinguni, kwenye miguu ya Yesu na Maria.

Nitasali kwa ajili ya Shirika letu ili liweze kuendeleza kazi kwa nia moja tu "kwa utukufu wa Mungu" na kwa ajili ya mema ya roho.

Wanangu wapendwa, jipeni moyo na iweni na imani!

Ingawa mwili wangu utakuwa kaburini, roho yangu na moyo wangu vitakuwa pamoja nanyi. Nawapenda na nawabariki. Endeleeni mbele kwa ujasiri mkifuata njia ile ile ya wema. Sursum corda! Mioyo yenu iwe juu! Kuweni na imani! Moyo wa Yesu upo pamoja nasi. Katika Moyo wake Mtukufu tumeunganika pamoja.